Posted 2022-07-08 07:27:44

Post By : Fr.Felix Mushobozi

WATATU WAPOKELEWA SHIRIKANI KWA DAIMA KAMA WAMISIONARI

Katika Parokia ya Mt. Andrea Mtume Bahari Beach, Siku ya Ijumaa Julai 1, ilikuwa siku njema, siku ambayo familia ya Damu Azizi inaadhimisha na kuheshimu thamani kuu ya Ukombozi wetu, wanafunzi wetu watatu: Alphons Martin Fataki, Bernard Hezron Kasambala na Faustine Barnabas Missanga, waliingizwa Shirikani kwa daima na hivyo kufanya idadi yetu kufikia tisini na wawili.

Mkuu wa Shirika Provinsi ya Tanzania Fr. Vedasto Ngowi ndiye aliongoza Misa Takatifu akishirkiana na Wamisionari zaidi ya ishirini. Wakati wa mahubiri yake Mkuu wa Shirika aliwahimiza Wamisionari wapya kuthamini hali yao hiyo mpya kama Wanashirika, akisema kwamba wao ni watu wa msalaba ambao Damu ya thamani Sana ya Bwana wetu Yesu Kristo inatiririka ili kutakasa ubinadamu wao na kuleta wokovu. Msalaba, ambao ni ishara maalum ya kuingizwa kwao Shirikani, ni ukumbusho wa wito na nguvu zao katika huduma yao wanayoianza.

Katika mahubiri yake yaliyoongozwa na masomo ya Misa, (Kut. 24:3-8; Efe. 2:13-20; Lk. 22:14-20), alibainisha umuhimu wa hatua hii ya maisha yao na kusema kuwa uamuzi wao si wa utani maana wanayakabidhi maisha yao yote kwa Mungu. Kama vile wana wa Israeli walivyoapa pale Mlima Sinai na damu ikawa ni ushuhuda, vivyo hivyo Wamisionari wapya wanajiweka chini ya ushuhuda wa Damu ya Kristo. Pd. Vedasto alikazia ukweli kwamba, kama Wamisionari wanapaswa kukumbuka kwamba wamepatanishwa na wakati huohuo wanapaswa kumleta Kristo ambaye amewapatanisha binadamu na Baba kwa njia ya Damu ya Azizi! Tumepatanishwa kwa damu ya Kristo. Sisi tuliotenda dhambi tumesamehewa! Sisi, ambao hatustahili upendo wa Mungu, tumeoshwa katika neema ya Mungu! Haijalishi ni dhambi gani, rehema ya Mungu ina nguvu zaidi! Mungu anaweza na anatupatanisha sisi sote kwa damu ya Kristo! Damu hiyo basi, iwe kwao kimbilio na nguvu kila mara wanapokumbana na changamoto mbalimbali katika Umisionari wao, Msalaba wa Bwana walioupokea kama ishara na utambulisho wao uwe kwao silaha na tegemeo.