Posted 2025-05-05 05:37:08

Post By : Fr.Felix Mushobozi

Fr. Emmanuel Amandi Kimoruru Amerudi kwa Baba

Fr. Emmanuel Amandi Kimoruru ameitwa kwa Baba yake wa Mbinguni ghafla mnamo Ijumaa Mei 2 2025 alipokuwa akisafiri kutoka nyumbani Moshi alikokuwa ameenda kwa mapumziko mafupi baada ya Shere za Pasaka. Sababu ya kifo chake inaonekana kuwa shinikizo la damu na sukari kutokuwa sawa. 

Kuzaliwa: Pd. Emmanuel Amandi Kimoruru alizaliwa tarehe 23 January 1961 Katika kijiji cha Kingachi Rombo. Wazazi wake ni Amandi Jacob Machamecha na Anna Saimoni Mshiki. Alibatizwa katika Parokia ya Usseri, tarehe 06 February 1961. Alipokea Komunyo ya kwanza tarehe 29 November 1971 katika Parokia ya Usseri na kupata sakramenti ya Kipaimara tarehe 11 March 1972 katika Parokia hiyo hiyo ya Usseri Rombo, Jimbo Katoliki la Moshi.

Elimu ya Awali: Fr. Emmanuel Kimoruru alipata elimu ya Msingi darasa la kwanza hadi la saba katika Shule ya Msingi Usseri, kati ya mwaka 1971 - 1977. Elimu ya Sekondari aliipata katika Shule ya Ufundi Moshi Technical School kati ya mwaka 1978 – 1981. Aliendelea na masomo ya kidato cha tano na sita katika Holy Ghost Seminary USA River kati ya mwaka 1982 – 1984.

MALEZI SHIRIKANI: Fr. Emmanuel Kimoruru aljiunga na malezi ya Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu kwa mwaka wa kwanza wa malezi terehe 15 Agosti 1986, kwenye nyumba ya Malezi ya Mt. Francisco Ksavery Itigi Singida. Ikumbukwe kwamba Pd. Kimoruru alijiunga na Shirika baada ya kumaliza masomo yake ya Falsafa  katika Seminari Kuu ya Mt. Anthony Ntungamo Jimbo Katoliki la Bukoba kati ya mwaka 1984-1986, akiwa Mseminari wa Shirika la Roho Mtakatifu (Holy Ghost). Fr. Emmanuel aliendelea na malezi ya kishirika na masomo ya Teolojia huko Roma Italia toka mwaka 1988 hadi alipopadrishwa.

DARAJA TAKATIFU: Fr. Emmanuel Kimoruru alipokea huduma ya Usomaji tarehe 26 February 1989 na huduma ya Utumikizi tarehe 26 October 1990 akiwa akiendelea na Masomo ya Teolojia kwenye Chuo Kikuu cha Mt. Thomas Aquinas Angelicum Roma Italia. Fr. Emmanuel Amandi Kimoruru alipokelewa Shirikani rasmi na kwa daima tarehe 07 December 1991 na kupewa daraja la Ushemasi tarehe 08 February 1992 katika Parokia ya Mwili na Damu Azizi ya Yesu Via Narni Roma Italia. Alipata daraja takatifu la Upadre tarehe 14 June 1992 katika Parokia hiyo hiyo.

UTUME: Baada ya Upadrisho Fr. Emmanuel Kimoruru alihudumu katika Seminary ya Shirika Mjini Roma akiwa Msaidizi wa Rector kati ya 1992 – 1993, na wakati huo huo alikuwa akichukua masomo ya Degree katika masomo ya Falsafa kwenye Chuo kikuu cha Kipapa cha Angelicum. Kabla ya kumaliza masomo hayo aliombwa kurudi Tanzania kwa utume na mnamo tarehe 7 July 1993 alipangiwa kufanya utume katika Parokia ya Damu ya Kristo Itigi kama Paroko msaidizi. Mwaka 1998 Fr. Kimoruru alihamishiwa katika Parokia ya Kintinku alikohudumu hadi mwaka 2008. Mwaka huo huo alikaa muda mfupi kwenye makao Makuu ya Shirika Kisasa na kuhamishiwa katika Parokia ya Bk Maria Mpalizwa Mbinguni Chibumagwa hadi Mwaka 2014. Pd. Kimoruru alihamishiwa katika Parokia ya Damu Azizi Tegeta akihudumu kama Msaidizi wa Paroko hadi Mwaka 2024 alipohamishiwa katika Parokia ya Kupaa Bwana Manyoni hadi umauti unamkuta.

UMAUTI: Pamoja na kwamba Fr. Kimoruru alikuwa na changamoto za afya zilizotokana na ajali ya gari mwaka 2009, kwa muda mrefu wa maisha yake alikuwa na afya njema ambayo ilikuwa ikimruhusu kufanya kazi za kitume, kiuchungaji na maendeleo ya jamii kwa bidii na ari kubwa. Umauti wake umemfika akiwa wa safarini kutoka nyumbani Moshi alikokwenda kwa mapumziko mafupi baada ya Sikukuu za Wiki Takatifu na Pasaka. Akiwa safarini siku ya Alhamisi, alipofika maeneo ya Katesh mkoa wa Manyara aliamua kupumzika kwa maana alijisikia vibaya. Jioni hiyo alipata huduma ya kwanza katika Kituo cha Afya cha Tumaini Katesh. Kesho yake alijisikia nafuu na kuomba msaada wa dreva ili afike Singida na hapo angeweza kukutana na dreva toka Manyoni ambaye angeendesha gari hadi Manyoni. Alipofika Singida, wakati wanasubiri dreva wa Manyoni afike, alizimia ghafla na hivi Mapadre wa Jimboni Singida walifika kutoa msaada wa kumpeleka Hospitali ya Tumaini Singida. Alipokuwa akipewa huduma ndipo umauti ulipomfika.

SHUKRANI: Tunamshukuru kwanza Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya maisha na wito wa Fr. Emmanuel Amandi Kimoruru. Mungu alimjalia karama nyingi njema alizozishiriki na watu wengi amabao waliishi na kufanya utume naye. Fr. Kimoruru alikuwa mcheshi, mchangamfu na mchapa kazi sana. Watu wote walioishi naye watamkumbuka kwa utayari wake kushirikisha karama alizojaliwa na Mungu hasa kazi za ufundi wa mikono yake na ukarimu wa kuwajali watu. Daima alitimiza wajibu wake katika Jumuiya kwanza kabla ya kuangalia mahitaji yake mwenyewe. Tunawashukuru watu wema waliomsaidia pale Katesh na kuhakikisha anaenda kulala mahali salama. Mwisho tunawashukuru Mapadre wa Parokia ya Katesh Jimbo la Mbulu, pia Mapadre wa Jimbo la Singida waliofika eneo la tukio alipozimia. Tunawashukuru pia wale waliousindikiza mwili wa Mpendwa wetu hadi Manyoni na kuuandaa kwa maziko.

 “Tuungane siku zote katika umoja mtakatifu wa mioyo na kila mmoja wetu amkabidhi mwenzake kwa Bwana, il kwa njia ya neema yake, kama tulivyoungana katika kwenye umoja wa utume, basi tena siku moja tuweze kuunganishwa naye katika Ufalme wake mtukufu ambao kwao kila siku tunafanya juhudi kuufikia” (Mt. Gaspari #1836).

MAZIKO:  Mwili wa Marehemu Pd. Kimoruru uliletwa Kanisani kwa Mkesha siku ya Jumanne jioni tarehe 6 May na Misa ya Maziko imeadhimishwa na Mhash. Askofu Edward Mapunda Askofu wa Jimbo Katoliki Singida. “Bwana alitoa, Bwana ametwaa, jina lake na lihimidiwe” (Ayubu 1:21).