Posted 2024-12-14 02:58:58

Post By : Fr.Felix Mushobozi

Merlini - Raia mashuhuri wa Spoleto mji uliomlea

[1] Raia Mashuhuri wa mji wa Spoleto na mji uliomlea

Na P. Michele Colagiovanni, c.pp.s.

Giovanni Merlini alizaliwa huko Spoleto (Italia ya katikati) mnamo tarehe 28 Agosti 1795. Alikuwa mtoto wa tatu kuzaliwa na baba Luigi na mama Antonia Claudia Arcangeli na kuzaliwa kwake kulipokelewa kwa sherehe kubwa. Furaha hiyo ilikuwa ya ajabu, kwani watu wote katika mji ule walikuwa wanajua jinsi wazazi wake walivyokuwa wakimsubiri kwa hamu kubwa. Luigi baba yake alitamani sana kupata mtoto atakayemrithi ili aheshimiwe kwa umaarufu na mali na kuleta utukufu katika ukoo mzima. Familia ya Merlini ilikuwa imesafiri kwa meli kutoka mbali hadi kwenye peninsula ya Italia miongo kadhaa ya miaka iliyotangulia, ikivuka Mlango-Bahari wa Messina kuelekea kaskazini. Wakati wa safari yao walienda wakitua katika vituo mbalimbali na kukaa kwa muda  mrefu au mfupi wakati wa safari iliyoonekana kutokuwa na mwisho.

Kadiri ya simulizi za Luigi familia yao ilikuwa ikiheshimika kama blazon. Baba yake Luigi alikuwa mtu maarufu wa koo muhimu katika mji wa Spoleto na alikuwa anajulikana kuwa ametokea Roma, kwa maana alikuwa ameishi kwa muda fulani pale na ndiko alikomuolea mke wake aitwaye Caterina Marzi tokea Viterbo. Alikuwa na wana kadhaa, ambao kati yao tunamfahamu Andrea, aliyezaliwa mwaka 1761, Luigi aliyezaliwa mwaka 1763, na mdogo wao Giovanni aliyezaliwa mwaka 1766. Hapo Spoleto ndipo kikawa kituo chao cha mwisho na makao yao ya kudumu. Nyakati zile mji wa Spoleto ulikuwa kama kituo mashuhuri, kama vile ulivyokuwa mkoa mzima wa Umbria, ambapo wasafiri walikuwa wakilazimika kupumzikia wakiwa kwenye safari zao. Kulikuwa na majumba na mitaa yenye heshima, makanisa mazuri, na kanisa kuu (Cathedral) la kifahari ambalo muonekano wake ulikuwa kama uwanja wa nyuma wa mraba unaoinamia chini kwenye kumbi za maonyesho. Muonekano wake ulikuwa kama vile watazamaji walioketi kwenye safu za mbele wanavyozuia mwonekano wa tukio kwa wale walio kwenye viti vya nyuma. Ni bayana kuwa katika uwanja huo hapakuwa na sofa au viti vilivyo pangwa kwa safu  ndiyo maana uwanja huo ulikuwa mtupu kama vile unasubiri kupangwa vile.

Ni dhahiri kwamba familia ya Merlini, kama ilivyo kwa watu wanaohamia mahali pageni walianza kujishughulisha ili kujipatia mahitaji yao. Tunaambiwa kuwa familia hii ilijipatia riziki zao kwa kutengeneza keki bidhaa ambayo ilihitajika sana wakati huo kama leo. Luigi alikuwa na ujuzi wa kutafuta mahitaji ya kiwanda hicho na mke wake Antonia Claudia Arcangeli aliweka vitu hivyo katika upishi kwa umahiri mkubwa, ili kila aina ya bidhaa ibaki katika ubora wake. Kwa muda mfupi biashara yao ilishamiri na nyumba yao ikawa kubwa na kuongezewa vitu vipya.

Luigi na Antonia wote walikuwa watu wa dini sana; hata hivyo, imani ya mwanamume huyo ilivutia zaidi, kwa sababu kiwango hicho cha imani kilikuwa adimu miogoni mwa wanaume wa wakati wake. Tunasimuliwa jinsi alivyokuwa na fadhila na imani ya kishujaa hasa katika uwanja wa ibada. Mfano ni wakati walipokimbilia kanisani kumwambia kwamba moto ulikuwa umezuka ndani ya nyumba yake, ukienea kutoka kwenye oveni ambayo ndiyo mapafu ya ustawi wa familia. Tunaambiwa kuwa Luigi alikuwa ametoka tu kupokea Ekaristi takatifu, akiwa njiani kurudi kutoka kwenye ukumbi wa kuabudia kwa ajili ya kutoa shukrani, badala ya kukimbilia nyumbani, kama vile mtu yeyote angefanya, bila shaka bila kujiletea lawama nyingi, alipiga magoti kwenye kiti cha kwanza kilichokuwa wazi, akitafakari huku kichwa chake kikiwa kimeegemea kwenye mikono yake kikishikamana na kingo na kisha, kwa mwendo wa kasi, akaenda kuthibitisha tukio hilo. Ni nje ya kanisa tu ndipo alianza kukimbia. Moto ulikuwa tayari umezimwa na uharibifu ulikuwa mwingi kuizidi jinsi mtu anavyoweza kukadiria. Utulivu huu wa kiibada wa Luigi hakuna aliyeusahau.

Baba mzazi huyu wa Giovanni Merlini alikuwa Mwenyekiti wa chama cha kitume cha Msalaba Mtakatifu, nafasi ambayo ni ya heshima na tunaambiwa alikuwa akitimiza vema majukumu yake. Pamoja na kasoro kadhaa alizokuwa nazo, alionyesha kwa vitendo alivyokuwa Mkristo na Mkatoliki kweli. Kila aliyetembelea nyumbani mwa familia ya Merlini  daima alikutana na harufu ya mikate na harufu hiyo ilibaki kwa muda wa masaa ishirini na manne na kuwafikia majirani. Ilionekana kuwa harufu ya nguvu isiyo ya kawaida, ambayo ni matokeo ya kufuata kwa uangalifu mapishi kadiri ya mapokeo kana kwamba yameandikwa kwenye kadi, kama vile maagizo ya kidini ya amri za Mungu na novena. Uwiano huo ulikuwa matokeo ya uzoefu wa karne nyingi, uliorithishwa kutoka kizazi hadi kizazi. Kila hatua ya mapishi na usindikaji ilichangia ubora wa bidhaa yenyewe.

Siku moja Givanni alimwomba baba yake ruhusa atengeneze kikanisa kidogo nyumbani mwao. Baada ya kutafakari kidogo baba yake alimruhusu, maana alijisemea, jambo la namna hiyo sio tu linaleta heshima katika familia lakini pia ni alama wazi ya utambulisho kwamba walikuwa raia wa himaya ya taifa la kipapa. Hivyo basi Giovanni alikigeuza chumba kidogo kikawa mahali patakatifu pa sala na kila aliyekiona chumba kile alitambua kuwa mtoto huyo ukubwani angekuwa fundi ujenzi. Wazo hilo liliyeyuka kwenye kichwa cha baba yake siku alipomueleza kuwa hamu yake ilikuwa ni kutoa maisha yake kama Padre. Wazo hili lilimkasirisha baba yake hata kufikiria kuwa mwanaye amepata matatizo ya kichwa, maana yeye hamu yake ilikuwa kumwona mwanaye kuwa mtu maarufu. Yeye Givanni aliwaza moyoni mwake kuwa hakuna heshima iliyo kuu zaidi ya kuwa kama Yesu yaani kuendeleza utume aliouacha duniani kwa kuwatumikia wengine. Ili kukabiliana na pingamizi hili kutoka kwa baba yake, wazo lililozunguka kichwani mwake ilikuwa ni kusali. Alimwomba Mungu ili wazazi wake wapate mtoto mwingine wa kiume, na sala zake zilisikilizwa, ndipo alipozaliwa mdogo wake aitwaye Petro. Hata hivyo baba yake aliendelea na msimamo wake wa kumkataza Giovanni kuwa Padre hadi mdogo wake huyo alipoanza kukua na kuonekana mwenye nguvu ndipo alipompa ruhusa ya kuingia seminarini.

Toka akiwa mvulana mdogo, Giovanni alitamani maisha ya utakatifu, na hakuna shaka kwamba hii ilionekana katika familia nzima na katika mji alimozaliwa. Jukumu la kuwa mtaratibu na mwangalifu halikuonekana kwake kuwa kizuizi cha uhuru wa kibinafsi, bali kwake ilionekana kama fursa ya kuodokana na pilika zilizosababishwa na fujo zisizotarajiwa. Aliamini kuwa ni vema ukiwa ndani ya nyumba unatafuta kitu na unaweza kukichukua ukiwa umefumba macho kwa kunyoosha mkono, kwa maana ndani yake kila kitu kimepangwa kwa utaratibu. Kwa jinsi mji ulivyokuwa nadhifu ndivyo hata majumbani mwa watu walivyokuwa. Wakazi wote wa mji kwake walikuwa kama sehemu ya familia na aliona kuwa ndivyo inavyostahili kuwa. Giovanni hakuwahi kuacha kushiriki shughuli za kijamii katika mji wake. Katika miaka yake ya kusoma shule kuna tukio moja ambalo lilibaki katika kumbukumbu zake kwa muda mrefu; nalo ni wakati baba yake alipobaki mbele ya Ekaristi takatifu hata baada ya kuarifiwa kuwa kulikuwa na moto ndani ya nyumba yao.

Katika miaka ile ambako Giovanni alikuwa akisoma seminarini kama mwanafunzi wa nje, kuna tukio ambalo lilimgusa kwa namna ya pekee na kubaki katika kumbukumbu zake. Siku moja akiwa darasani na wenzake, wakati mwalimu alipokuwa hayupo darasani, kulitokea fujo kati ya wanafunzi na wakaanza kurushiana vitu –  daftari, rula, vitabu nk. Kitu fulani kikatua kwenye dirisha na kuvunja kioo chake. Mwalimu aliporudi na kuuliza nani alikuwa amesababisha kuvujika kwa kioo kile, ilisikika sauti ya mmoja wao ikimtaja Giovanni na baadhi wakiashiria kukubaliana naye. Hata hivyo Giovanni baada ya kutafakari kidogo alimwambia mwalimu kuwa wanaonituhumu si ajabu wako sahihi maana, hata kama sikuvunja mimi au kusababisha fujo, sikuwajibika kuhalikisha tukio kama hilo halitokei. Baada ya miaka mingi, Pd. Henrico Rizzoli, ambaye ndiye aliyefuatia kama Mkuu wa Shirika, alisema kuwa tukio hili linatuonyesha jinsi Giovanni alivyokuwa mnyofu na mwenye kutafuta daima ukamilifu. Hiki ndicho alichomaanisha, na kuanzia siku hiyo akazidisha juhudi zake za kujua jinsi ya kuchangamkia fursa na kujitahidi kuwa mwema zaidi na zaidi. Kwa kujishughulisha kwa bidii, Don Giovanni Merlini alifikia kiwango cha juu cha ukamilifu. Pd. Enrico Rizzoli alitoa hoja kwamba sio rahisi kuona watu wa kiwango cha juu cha muungano na Mungu kama alivyokuwa Giovanni Merlini.

 

[1] Makala hii ilichapishwa kwenye Gazeti “Nel Segno del Sangue”, May/June 2019. Imetafsiriwa kwa Kiswahili na Fr. Felix Mushobozi, c.pp.s.

blog-img