Posted Mon Dec 2024
Post By : Fr.Felix Mushobozi
KIKOMBE CHA DAMU YA AGANO JIPYA
UTANGULIZI:
Ni wiki la Damu Azizi ya Bwana – Mwaka huu 2023 tunatafakari juu ya Tasaufi ya Damu Azizi tukiangalia alama ya KIKOMBE. Miaka miwili iliyopita tulianza kutafakari juu ya Agano, mwaka jana tukatafakari juu ya Msalaba na Mwaka huu ni juu ya Kikombe. Kama tulivyosikia jana na juzi kwenye Misa ya ufunguzi, Tasaufi yetu inaeleweka kama tutaelewa alama ambazo zimetumika katika Biblia, Mapokeo, Taalimungu (Teolojia - Tauhidi) na maisha yetu ya kila siku. Kuna ishara nne zinazotoka katika tasaufi yetu, nazo ni: Agano, Msalaba, Upatanisho na Kikombe. Sisi sote ni watu wa Agano, watu wa msalaba, watu waliopatanishwa na watu wa kikombe. Sisi sote tumekombolewa kwa Damu ya Kristo.
Kutokana na muda tulionao hatuwezi kueleza kiundani KIKOMBE CHA AGANO JIPYA ila mawazo kadhaa ambayo yatatuongoza kuelewa Teolojia ya Kikombe cha Agano Jipya.
Katika Mila na desturi za watu wote hamu ya kuishi katika ushirika na miungu ni kitu cha siku zote. Wengi hufanya jitihada za kufikia lengo hili kwa njia mbalimbali. Kutolea sadaka wakitumia vyakula au vinywaji na vitu vingine ambavyo mwanadamu anavitumia katika maisha yake ya kawaida. Walitumia pia viwakilishi ambavyo waliamini vinawakilisha miungu yao, kama vile milima, mito, maziwa, bahari miti, wanyama kn. Wayahudi katika Agano la Kale waliona uwepo wa Mungu wao katika Mlima Sinai na ndiko walipofanya naye Agano. Hatuna haja ya kuingia katika Agano la Kale kwani jana tulisikia jinsi Kikombe kilivyotumika katika mahusiano kati ya Israeli na Mungu wao.
Katika Agano jipya Yesu Kristo ndiye Mshenga kati ya Mungu na mwanadamu. Katika Agano la Kale tulisikia jinsi Mwanadamu alivyokuwa anahusiana na Mungu sio kwa ukaribu, tena asingthubutu kumkaribia Mungu. Katika Yesu Kristo ushirika na Mungu umewezekana kwa kuwa yeye ameshiriki ubinadamu, hata katika udhaifu (2Pt 1,4; Ebr 2,14), isipokuwa hakutenda dhambi.
Jumuiya ya Wafuasi wa kwanza wa Kristo walionyesha ushiriki wao kwa Kikombe cha ushirika kwa kujenga umoja wa wana Kanisa. Hii ilidhihirika katika maisha ya Jumuiya ya kwanza ya Wakristo. Wakristo wa kwanza waliishi Kikombe cha ushirika kwa kuishi amri kuu ya Upendo, kwa imani na matumaini wakitoa ushuhuda wa kumfuasa Kristo. Hali hii ilionekana kila mara walipokusanyika “kuumega Mkate” (Mdo 2,42) na kushirikishana mahitaji yao ya kila siku (Mdo 4,32) na hivi waliishi kwa mshikamano (Rm 12,13; Gal 6,6; 2Kor 8,4;Ebr 13,16). Mshikamano huo ulionekana zaidi hasa wakati wa dhiki na madhulumu, wakiishi kwa pamoja na kutiana moyo (1Kor 1,7; Ebr 10,33; 1Pt 4,13) Moyo huo wa ushirika uliwasaidia kueneza habari njema (Fil 1,5).
Ushirika huo ulikuwa wa kina: Wakristo wa Kwanza waliishi kikombe cha ushirika sio katika mambo ya nje tu, bali ushirika wa Roho na kweli. Maana Mkristo alibatizwa na kwa tendo hilo aliifia dhambi katika Kristo na kufufuka naye katika maisha mapya (Rm 6,3-14; 2Kor 4,14; Rm 8,17; Fil 3,10k; 1Tes 4,14). Ushirika huu wa kina na Mwana wa Mungu uliwezekana kwa njia ya kushiriki kwenye mwili wa Ekaristi (1Kor 10,16) yaani Kikombe cha ushirika. Lakini ushirika huo unawezeshwa na Roho Mtakatifu (2Kor 13,13; Fil 2,1).
Kikombe cha Ushirika kadiri ya Mtume Yohane ni ushirika na Baba na udugu kati ya Wakristo (1Yn 1,3). Ushirika huu ni Kukaa = kubaki, kama vile Baba na Mwana walivyo wamoja; yaani Baba anakaa ndani ya Mwana na mwana anakaa ndani ya Baba katika pendo, viyo hivyo Wakristo wakae katika pendo la Baba na la Mwana kwa kushika amri zake (Yn 14,20; Yn 15,4.7; 17,20-23; 1yn 2,24; 4,12).
Ushirika wa namna hii unawezekana tu kwa msaada wa Roho Mt. (Yn 14,17; 1Yn 2,27; 3,24; 4,13). Ekaristi Takatifu ni Chakula cha wasafiri kinachowawezesha wafuasi wa Kristo kuishi katika muungano huo wa ndani na wa kudumu: “Aulaye Mwili wangu na kuinywa damu yangu, anakaa ndani yangu nami ndani yake” (Yn 6,56).
Mkristo kwa kushiriki Kikombe cha ushirika na Bwana, anaonja kabla ya wakati ile furaha isiyo na mwisho, ambalo ni tamanio la kila moyo wa mwanadamu, ambalo ndilo lililokuwa tumaini la Israeli – yaani kuishi na Mungu milele (1Tes 4,17; Yn 17,24).
“Malaika wa tatu akawafuata hao wawili akisema kwa sauti kubwa, “Kama mtu yeyote anamwabudu huyo mnyama na sanamu yake na kutiwa chapa yake kwenye kipaji chake cha uso au kwenye mkono wake, yeye pia atakunywa mvinyo wa hasira kali ya Mungu ambayo imemiminwa katika kikombe cha ghadhabu yake pasipo kuchanganywa na maji. Naye atateswa kwa moto uwakao na kiberiti mbele ya malaika watakatifu na mbele za Mwana-Kondoo”. (Ufu 14,9-10;15,7—16,19).
Sadaka hiyo ni Kikombe ambacho Baba alimpa Mwana akinywe, kama anavyothibitisha Mwinjili Yohane: “Simoni Petro, aliyekuwa na upanga, akaufuta na kumkata sikio la kuume mtumishi wa kuhani mkuu. Jina la mtumishi huyo aliitwa Malko. Yesu akamwambia Petro, ‘Rudisha upanga wako kwenye ala yake. Je, hainipasi kukinywea kikombe alichonipa Baba?” (Yn 18,10-11). Kwa utii wa kimwana, Yesu anakipokea kikombe hicho kwa ajili ya wokovu wa watu! Anakinywea kikombe hicho kwa niaba (kwa ajili) ya wote watakaokombolewa na anamshukuru Baba (Mk 10,39).
NB. Katika nyakati zote, Kikombe hiki ni kikombe cha wokovu, kama anavyothibitisha Mzaburi: “Nitainua Kikombe cha wokovu na kuliita jina la Bwana” (Zab 116,13). Kikombe hiki ni kikombe kwa ajili ya watu wote wanaoshiriki katika Damu ya Kristo hata atakapokuja tena. Kwa kushiriki kikombe hiki wanapewa ruhusa kumbariki / kumtukuza Mungu ambaye atawakaribisha kukunywea kwenye meza ya Mwanaye katika Ufalme wake!
Yesu mwenyewe anabainisha kuwa Karamu hiyo aliyokula na Wafuasi wake, ulikuwa ni wakati muhimu kihistoria. Ishara na maneno aliyotumia Yesu wakati wa Karamu hiyo yalikuwa na maana kubwa sana. Ni Karamu mama wa Karamu zote. Ni Karamu ambayo tukitaka kuelewa tunayofanya leo katika Ekaristi Takatifu na katika Sakramenti ya Daraja, lazima kuielewa vizuri Karamu ya Bwana. (Ni Hermeneutic event – Funguo za tafsiri).
MANENO YALIYOTUMIKA KWA KIKOMBE: Marko na Matayo wanasisitiza Maneno: “Hii ndiyo Damu yangu ya Agano itakayomwagika kwa ajili ya wengi” (Mk 14,24) na Matayo anaongezea “kwa maondoleo ya dhambi” (Mt 26,28).
Luka na Paulo 1Kor wanatumia: Kikombe hiki ni Agano jipya katika Damu yangu imwagwayo kwa ajili yenu” (Lk 22,20; 1Kor 11,25).
Maneno yaliyotumika katika Misale ya Misa yanachukua kutoka Mapokeo yote mawili: “TWAENI MNYWE NYOTE, HIKI NDICHO KIKOMBE CHA DAMU YANGU, DAMU YA AGANO JIPYA NA LA MILELE, ITAKAYOMWAGIKA KWA AJILI YA WENGI, KWA MAONDOLEO YA DHAMBI”
Maneno mengi yanachukuliwa kutoka kwenye Mapokeo ya Marko na Matayo; kutoka Luka na 1Kor yalichukuliwa maneno: “kwa ajili yenu” na “Agano jipya”.
Katika mafundisho ya Paulo Kikombe hicho kimeitwa “Kikombe cha Baraka”: “Kikombe cha Baraka = kikombe tunachokibariki je, si ushirika katika damu ya Kristo?” (1Kor 10,16). Kikombe anachokiongelea Paulo ni kile ambacho kinanywewa baada ya kusema sala ya Baraka. Ni tofauti na lile bakuli / Kombe ambalo ndani mwake iliwekwa damu ya kunyunyizia Altare.
Kikombe ambacho kimekuja kujulikana katika Ekaristi Takatifu ni kile Kikombe cha Wokovu tulichokiona hapo mwanzo, kilichotajwa katika Zaburi 116,13. Huu ni wimbo uliotumika katika Karamu za Pasaka ya Kiyahudi ziitwazo HILLEL.
Maana ya ndani ya Kikombe katika Biblia ni (DESTINY = Ukomo ulioandikiwa). Ni katika maana aliyotumia Yesu alipowajibu Wana wa Zebedayo: “Mwaweza kukinywea Kikombe nitakachonywea mimi na kubatizwa Ubatizo nitakaobatizwa mimi?” (Mk 10,38). Ni katika maana hiyo hiyo tunayoikuta katika Sala ya Yesu pale Getsemane: “Abba, Baba, yote yawezekana kwako, uniepushe Kikombe hiki, lakini si nitakavyo mimi, bali utakayo Wewe” (Mk 14,36).
Yesu ameenda kupokea mateso ambayo ni Kikombe kichungu, walichomwandalia wanadamu, wakimhukumu kwa sababu ya utii wake kwa mapenzi ya Baba. Katika Ekaristi hakuna Kikombe cha hasira / gadhabu, bali kwa kukubali mapenzi ya Baba anakutana na majaribu yanayosababishwa na uovu wa mwanadamu. Kadiri alivyojikabidhi katika upendo wa Baba ndivyo Baba alivyomwokoa (Yn 12,27).
NB. Hivyo basi kukinywea kikombe maana yake ni kuungana na Kristo katika ushirika aliokuwa nao na Baba wakati anakubali kujitoa kafara, wakati wa mateso na mahangaiko makuu.
NB. Agano ambalo linaunganishwa kwenye Kikombe cha Ekaristi linaitwa “JIPYA”. Agano hili ni lile lililobatilisha la zamani ambalo Manabii walilitabiri. Historia ya Israeli inathibitisha jinsi ilivyokuwa vigumu kushika Agano la zamani = Sheria – Torati; kwani mara nyingi watu walilishika kwa nje tu katika ibada. Manabii walikuwa wakitumaini Agano Jipya kama inavyoshuhudiwa na Yeremia (31,31-34). Mungu anaahidi kuandika maneno yake katika mioyo. Katika Ezekieli (36,24-28) Agano Jipya linaahidiwa kuwekwa kwa njia ya karama ya Roho mpya. Agano hili jipya ni la “milele” (Mw 9,16; Is 55,3). Usemi huu wa Agano jipya na la milele una chimbuko lake katika maandiko haya.
Agano hili jipya ni katika Damu ya Yesu kama anavyoshuhudia Luka na Paulo 1Kor. Hivyo basi Agano analoratibisha Yesu liko katika NAFSI YAKE – katika MAISHA yake. Na hivi kutimiza Agano sio katika kutenda maneno / Sheria bali katika muungano na nafsi ya Yesu anayelifunua na kulitimia ambaye inampasa kila anayemwamini kumfuasa. Yesu ni NENO, maneno yote aliyoyanena Baba yametimia katika Yeye.
NB. Kukinywea Kikombe cha Agano jipya ni kukubali Mpango / Agano jipya katika Yesu na kuwa tayari kuongozwa na Roho Mtakatifu ambaye ndiye anayetimiza yote katika nafsi ya kila mmoja na katika kila Jumuiya. Jukumu letu ni kushuhudia uhusiano huu mpya na Mungu.
Damu ya Yesu iliyomwagwa ni kitendo cha kikatili, cha chuki ambayo wanadamu waliamua kufanya ili kumkomesha, sababu ya chuki waliyokuwa nayo. Kifo cha Yesu sio Mapenzi ya Baba, Mapenzi yake ni kuwa atomize kazi aliyomtuma Mwanaye. Ili nia hii itimie ilimpasa Yesu apambane na upinzani huo katili.
Yesu alikubali kufa ili kuonyesha utii kwa utume aliokabidhiwa na Baba yake, kuonyesha kuwa Karama za Mungu haziwezi kudharauliwa kwa ugumu wa mioyo. Kikombe ni ishara ya tendo hili kuu. Tendo hili, japokuwa ni la kusikitisha, laonyesha jinsi mwanadamu asivyo na shukrani. Sio janga bali ni fursa ya kutoa ushuhuda wa maisha mapya katika Yesu na jinsi yalivyopokelewa. Kama zawadi ya Baba, licha ya mateso na kifo, Yesu anayapokea maisha haya mapya katika Roho Mtakatifu, na kuwakirimia walio wake. Ndio maana hata kabla ya kifo chake Yesu anamshukuru Baba.
NB. Kukinywea kikombe cha Ekaristi ni kuridhia kwa upendo na shukrani mapenzi ya Baba, kwa kupitia Yesu aliyetuonyesha utii na uaminifu wake kwa Baba hadi upeo wa Kifodini / Matyrdom. Kila tukinyweapo kikombe hiki tunaahidi kuwa kama Yeye – waaminifu kwa neon ambalo Mungu anatufunulia kama Mapenzi yake. Ni kutambua thamani na ghrama ya Upendo wa Mungu, tukishukuru na kutumaini katika maisha mapya tuliyokirimiwa na Mungu, licha ya makandokando yetu yenye dalili za kifo, tunayoyakalibili kwa hiari na upendo mpaka uzima usio na mwisho, ambao kifo hakiwezi kutuondolea.
Luka anatumia “kwa ajili yenu” akimaanisha – kwa ajili ya wafuasi wake. Marko na Matayo wanatumia “kwa jili ya wengi”, na katika lugha ya kiBiblia inaeleweka “kwa ajili ya wote”, bila kuonyesha kuwabagua wengine. Ndiyo maana kwa muda mrefu, formula iliyotumika katika Liturgia zetu za Ekaristi ilikuwa ni “kwa ajili ya wote”.
Kwa muda mrefu kumekuwa na mjadala kati ya Wataalamu wa Biblia juu ya maana halisi ya “KWA AJILI YENU”. Kwa muda mrefu ilieleweka kwamba Yesu alimwaga Damu yake “Kutulipia” dhambi zetu na za dunia nzima. Damu ya Kristo ilionekana kama ni “Malipizi”, kana kwamba Mungu alitulizwa hasira yake kwa Damu. Kwa sasa Wataalamu wa Biblia wa siku hizi wanatafsiri “kwa ajili yenu” kuwa ni “Kutusaidia” – “kutuhudumia”, kutupa nguvu ya kuhudumia. Sababu ya uelewa huu ni kwamba maisha yote ya Yesu duniani aliyaweka kwa kutuhudumia sisi ili tupate wokovu na kwa ajili ya wokovu wa dunia nzima. “Kwa maana Mwana wa Mtu hakuja kutumikiwa, bali kutumikia na kutoa maisha yake kuwafidia wengi” (Mk 10,45).
Utume wa Yesu hadi mwisho wa maisha yake hapa duniani (kwa kifi cha hiari na upendo) yalikuwa ni huduma ili kuufaidia ulimwengu katika mtindo wa utumishi. Ndiyo maana katika Karamu ya mwisho, Yesu anaonyesha ishara ya utumishi huo: Japokuwa Yeye ni Bwanana Mwalimu, yeye aliwaosha wafuasi wake miguu ili nao waige mfano, watende kama yeye alivyowatendea (Yn 13,13-15). Mwinjili Luka baada ya simulizi la Karamu ya mwisho anamalizia kwa kusema: “Lakini mimi nipo hapa miongoni mwenu kama mwenye kutumikia” (LK 22,27). Mwinjili Yohane naaposimulia tendo la Yesu kuwaosha miguu wafuasi wake, ana lengo la kuonyesha maana halisi ya Ekaristi Takatifu. Hivyo basi Ekaristi yatudai utumishi – kuoshana miguu; na Kanisa ni Jumuiya ya wanaotumikia, “Watumikizi”!
HITIMISHO:
NB. Kifo cha Yesu ni kweli ni fidia kwa dhambi zetu, lakini sio katika maana ya kipagani – kwamba Mungu alihitaji Damu ya Mwanaye ili tupewe msamaha[3], bali kwamba Utii wa Yesu kwa Baba hata kifo cha msalaba kilikubalika mbele ya Baba kuliko hasira yake iliyosababishwa na dhambi zetu! Ndiyo maana kushiriki Komunyo Takatifu ni tendo la kujiapiza! Ndio maana Paulo, kwa sababu hiyo anawaonya Waamini wa Korinto: “Kwa hiyo kila aulaye mkate huu au kukinywea kikombe cha Bwana katika hali mbaya anakufuru Mwili na Damu ya Bwana. Basi mtu ajihoji dhamiri kabla ya kuula mkate na kukinywea Kikombe. Maana mwenye kula na kunywa bila kufanya tofauti kati ya Mwili na chakula cha kawaida, anajilia na kujinywea hukumu” (1Kor 11,27-29).
Basi, kuna umuhimu wa wa kujiandaa vema kabla ya kupokea Mwili na Damu ya Bwana: kuchunguza dhamiri, kutubu na kuongoka. Upyaisho wa namna hii wawezekana kwa njia ya Roho Mtakatifu.
Kukinywea Kikombe cha Agano jipya ni kuonyesha uhitaji wa kupokea msamaha wa dhambi zetu, kupatanishwa na Mungu na kuahidi kujitahidi kutembea katika safari ya wongofu na upatanisho na ndugu zetu!!
[1] Maudhui haya yametoka kwenye Makala ya: Xavier Léon-Defour (Ed), Cup, in Dictionary of Biblical Theology, Article by Peirre-Emile Bonnard, pg 85, Geoffrey Chapman London, 1972. Article by Daniel Sesboúé & Jacques Guillet, Communion, Ibd. Pg. 69-71.
[2][2] Tafakari zifuatazo na maudhui yake, chimbuko lake ni chapisho la Luigi Della Torre, BERE AL CALICE EUCARISTICO, lilichapishwa katika QUADERNI SANGUIS CHRISTI # 10, Pia Unione Preziosissimo Sangue (Ed), Roma, 1984.
[3] Jaribu kufikiria Ibrahimu alipoagizwa na Mungu kwenda kumtoa sadaka Mwanaye wa pekee Isaka. Pamoja na kwamba alikuwa na uchungu mkubwa moyoni, alitii kwa Imani kuu! (Mw 22,9-14). Toka wakati huo Mungu anapiga marufuku rasmi kafara ya binadamu kama ilivyokuwa desturi ya Wakaanani.
Posted Mon Dec 2024
Post By : Fr.Felix Mushobozi
TOKA BARUA ZA MWENYEHERI YOHANE MERLINI
“Ndugu zangu, tunahitaji kuwa na Moyo mkuu, kwa sababu ya hali ya nyakati tunazoishi; na si kwa ajili yetu tu, kwa ajili ya kurekebisha kasoro zetu na maendeleo katika kudumu kwenye njia za Bwana, lakini pia zaidi ya yote kwa ajili ya watu wengi ambao, amabao wanajiachia na kupofushwa na maovu, wanaotembea kwa kasi kuelekea uharibifu wa milele. Tunahitahi hili ili kuwatikisa na kuwakumbusha umuhimu wa Neema. Lakini ni wapi tunakoweza kwenda kupata roho hii kama si katika tanuru isiyozimika ya Moyo wa kimungu? Tunawasiliana katika kiini hiki cha fumbo, kwa sababu hapa tunapata Mvinyo wenye uwezo wa kutupatia divai iliyo dawa pekee inayoweza kuponya magonjwa yetu. Ni divai ya ukarimu, pekee ambayo inaweza kuimarisha nguvu za roho zetu; divai yenye nguvu, ndiyo pekee inayoweza kutufanya tuwe na nguvu ya kukua katika fadhila na wema. Ndiyo divai, hatimaye, ya uaminifu wa mbinguni, divai pekee yenye ufanisi katika kututia nguvu mioyoni mwetu... Katika chumba hiki cha ndani na kwa Divai hii Bwana atatusaidia na kutufariji! Tunamsihi sana mpendwa wetu Yesu awe tayari kutumia tunda la Damu ya kimungu kwetu. Hivyo basi tutashiriki katika Roho wake yuleyule: Roho wa ukamilifu kwa ajili yetu, Roho wa bidii kwa ajili ya heshima ya Mungu, Roho wa upendo kwa ajili ya wokovu wa roho”[1].
Kama wanafunzi wa kwanza wa Yesu, ndivyo alivyokuwa Giovanni Merlini: mtakatifu, kwa kweli, ndiye anayejua jinsi ya kuishi mang’amuzi halisi wa ufuasi wa Yesu. Katika mistari hii, Mwenyeheri wetu anatufunulia ukweli ambao kwa namna fulani ni wa kutatanisha, wa kustaajabisha: tunafikiri, kwa hakika, kuhusu Mmisionari wa Damu Azizi kama mtu asiye na makao maalum, mhamaji wa Injili ambaye haweki mizizi kabisa mahali popote kwa sababu amekubali kuwa mhudumu asiye na makazi kwa maisha yake yote.Merlini kama muasisi wa Shirika letu anataka kutuonyesha nyumba ambayo hakutaka kutoka kamwe na anatualika kuingia, kubaki, kunywa na, zaidi ya yote, kuishi ndani yake ...
Kwa hiyo basi, huyo Mmisionari ana makao ya kudumu na makao yenyewe ni Moyo wa Yesu Kristo! Humo ndimo Giovanni Merlini alimopata siri ya mafanikio ya kitume, ya kuongoza Shirika na kutunza roho nyingi za watu. Katika moyo huo Mtukufu Merlini aliweza kutembea katika njia za ulimwengu huu bila hata kuiacha nyumba hiyo. Merlini anaandika maneno haya kwa Wamisionari wenzake moja kwa moja kutoka kwenye moyo huo, akitumaini kwamba wao pia hawataiacha kamwe nyumba hiyo. Merlini daima amekuwa na mtazamo wa kujua kwamba, kama ilivyokuwa hatari kwa watu wa wakati wake, kutegemea nguvu ya kibinadamu, ndivyo ingekuwa mara mia katika 2019. Hatari yenyewe ni ile ya kuzingatia ufanisi ulio matunda ya fikra za ulimwengu huu ambazo hutupeleka nje na hata mbali ya Moyo wa Yesu. Matokeo yake ni maisha ya kiroko kupungua. Tunalitambua hilo tunapohangaika, nguvu na mawazo yetu yanapopungua, tunapohangaika kutafuta furaha katika maisha yetu ya sasa, upendo unapokuwa mgumu... Kwa wakati huo tunarudi kujiuliza: Mwalimu anaishi wapi? Swali hili ndilo njia ya uzima ambayo daima itaturudisha kwenye Moyo ule ambao peke yake unaweza kutupa damu ya uhai, dawa, nguvu na uaminifu, hisia sahihi, na ambazo ni silaha ya daima dhidi ya kila kitu kinachozuia Uhai: ndiyo Damu Azizi ya Yesu Kristo.
[1] Yohane Merlini, Circular Letter n. 18, uk. 62.