Posted 2024-07-11 16:43:51
Post By : Fr.Felix Mushobozi
Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu Province ya Tanzania, ina furaha kubwa mwaka huu 2024 kwa kupata vijana tisa walioamua kujiunga na Shirika kwa maisha yao yote. Vijana hao wamepokelewa Shirikani wakati wa adhimisho la Misa Takatifu iliyoongozwa na Mkuu wa Shirika Province ya Tanzania Pd. Vedasto Ngowi. Tukio hilo limefanyika jioni ya tarehe 01.07.2024 katika Parokia ya Damu Azizi ya Yesu Tegeta, jimbo kuu la Dar es Salaam. Vijana hao ni Frt. Abias Mkwetu Thadeo, Frt. Alphonce Gervas Lang’u, Frt. Andrew Nicholas Mauya, Frt. Cyprian Juma Damian, Frt. Deogratias Ismail Dimosso, Frt. Erasmo Lazaro Mligo, Frt. France Rwehabura Chrizostomu, Frt. Metodi Pastory Kibiriti na Frt. Wilberd Joseph Chuwa.
Aidha katika adhimisho hilo la misa, Mkuu wa Shirika alitukumbusha kuwa katika siku ya kwanza ya mwezi wa saba katika kalenda ya Shirika kwa hapa Province ya Tanzania imewekuwa ni desturi sasa kuwapokea rasmi na daima vijana wanaojiunga na Shirika. Amewakumbusha vijana hao kwamba kwa kujiunga na Shirika wanawekwa wakfu kwa Kanisa, wanakuwa mali ya Kanisa na Shirika. Utume wowote watakao ufanya ni kwa ajili ya Kanisa na Shirika. amewakumbusha pia katika utume wao kwa Shirika, kutakuwa na kufanikiwa, kushindwa, kuanguka, kuinuka, kupigiwa makofi na kukataliwa. Wajiweke tayari kwa hayo yote. Lakini mwisho daima wamtazame Kristo wanayemfuata. Wanapopitia katika utume mgumu au vipindi vigumu daima wamtazame Kristo ambaye ndiye wanayemfuata na amepitia hali zote. Mkuu wa Shirika pia aliwaita vijana hao kwa jina la “Vijana wa Merlini”, kwa kuwa itakumbukwa kuwa hivi karibui Kanisa litapa zawadi ya kutangazwa Mwenye heri Mtumishi wa Mungu Yohane Merlini, ambaye amefanya mambo mengi na makubwa sana katika Shirika la Damu Azizi. Amewataka kuiga na kufuata mfano wa Yohane Merlini kwa kujibidisha kutenda yale wanayopaswa kuyatenda tena kwa kiwango cha juu kabisa cha akili, karama na vipaji vyao walivyojaliwa na Mungu.