Posted 2022-07-08 08:08:43

Post By : Fr.Felix Mushobozi

WAMISIONARI WAPYA WATATU WAPEWA DARAJA LA USHEMASI

Siku iliyofuata Incorporation, Jumamosi Julai 2, palepale Parokiani Bahari beach, Wamisionari wapya waliwekwa wakfu na kuwa Mashemasi katika adhimisho la Misa takatifu iliyoongozwa na Mhash. Ask. Stephano Msomba, OSA. Wengi wa Wamisionari wa CPPS kutoka District ya Dar es salaam na mapadre kutoka sehemu mbalimbali walihudhuria. Watawa wengi wa kike na kiume, wakiwemo Masista wa ASC walishiriki.

Wakati wa mahubiri yake Askofu Msomba, alijikita katika maudhui ya mistari miwili ya Injili ya Yohana: “Kama vile Baba alivyonipenda mimi, mimi nilivyowapenda ninyi; kaeni katika pendo langu”. (Yn. 15, 9) na “Hii ndiyo amri yangu, kwamba mpendane kama nilivyowapenda ninyi”. (Yn.15, 12). Askofu Msomba aliwaasa mashemasi hao watatu kuishi kwa kufuata mfano wa Kristo ambaye amewapenda wananadamu upeo. Aliwataka watambuliwe kwa upendo wao kwa Kristo na watu wake. Ushahidi wao wa maisha waliofunzwa katika miaka yao mingi ya malezi lazima ubainishe maisha na huduma watakazotoa kwa Taifa la Mungu. Aliwaonya wasifikirie kuwa kwa kupewa daraja hilo wamefikia lengo lao; aliwataka waendelee na mchakato wa malezi endelevu ambayo lengo lake ni utakatifu. Kwa ustahimilivu na unyenyekevu wao inabidi waendelee kumtumaini Mungu pekee na si katika malimwengu. Aliwaasa kuwa tayari kujifunza na kupokea mashauri kutoka kwa wengine, alihitimisha. Baada ya adhimisho la Ekaristi takatifu yalifuata maakuli na shangilio yaliyotayarishwa na Wana Parokia ya Bahari Beach kwa ukarimu, licha ya changamoto ya kunyesha kwa mvua kubwa.