Posted 2021-05-16 04:38:28

Post By : Fr.Felix Mushobozi

Ombi la Pd. Deogratias Baharia kujiunga na CPPS Tanzania

Mnamo mwezi Januari mwaka 2021, tulipokea ombi kutoka kwa Pd. Deogratias Baharia wa Jimbo la Morogoro kujiunga na shirika letu. Baada ya mawasiliano baina yake na Mkurugenzi wa miito, kisha na Padre Provincial na Council, pamoja na Msimamizi wa kitume wa Jimbo la Morogoro ombi la Pd. Baharia lilikubaliwa.

Padre Baharia mpaka sasa alikuwa Paroko wa Parokia ya Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni Kinda. Kabla ya kumruhusu Pd. Baharia kuanza rasmi mwaka wa malezi, Msimamizi wa Kitume Pd. Lazarus Msimbe SDS, aliomba apewe muda wa kutafuta paroko. Baada ya muda alifanya mazungumzo na Padre Provincial na kueleza ugumu wa kumpata paroko. Hivyo aliomba Shirika likubali kuchukua parokia na kutoa huduma. Hili lilikuwa ni ombi la ghafla na ambalo halipo kwenye mpango wetu. Baada ya mazungumzo na majadiliano, tukijali pia hitaji la huduma kwa waamini wa Kinda, tumemkubalia Msimamizi wa Kitume kutoa huduma kwa kipindi cha mwaka mmoja. Aliomba kama haiwezekani kupokea utume huo moja kwa moja basi walau kwa muda mfupi.

Parokia ya Kinda ipo Milimani katika Wilaya ya Mvomero. Pamoja na parokia, kipo pia kituo kipya cha Kiroho kiitwacho Totus Tuus. Kina vyumba takriban 50, ukumbi, kanisa la kuabudu, nk. Kuna mazingira mazuri ya utulivu. Kituo hiki kimejengwa kwa ufadhili na wafadhili binafsi wa Pd. Baharia. Msimazi wa kitume alituomba pia tukichukue kituo hicho. Changamoto iliyopo ni barabara yenye urefu wa Km 6 hasa msimu wa mvua kwani ni mlimani.

Baada ya kutafakari, na kwa kuzingatia mandhari ya eneo la Kinda, tuliona kwamba panafaa pia kwa malezi. Pd. Achileus Mutalemwa atakuwa paroko kwa kipindi hicho. Tayari Mons. Lazarus Msimbe SDS, amemteua Pd. Achileus kuwa Paroko kuanzia tarehe 10 Mei 2021. Pia atahamia Kinda pamoja na vijana wa mwaka wa pili wa malezi. Tunaendelea kuangalia namna ya kusaidiana naye katika utume huo mpya. Tayari Padre Provincial, Makamu wa Provincial na Pd. Achileus mwenyewe walishafika huko Kinda kusudi kuona mazingira na kuamua. Kipindi hiki cha mwaka mmoja kitakuwa pia kipindi cha “majaribio”. Baada ya kipindi hicho tutafanya tathmini tujue nini cha kufanya.

blog-img