Posted 2021-03-19 04:40:55
Post By : Fr.Felix Mushobozi
JUBILEI YA MIAKA 25 YA SEMINARI YA MT. GASPARI; NDOTO INAENDELEA
Mt. Gaspari alikuwa na ndoto ya kueneza upendo wa Damu ya Yesu popote Duniani. Ndoto hiyo ilidhihirika tarehe 15/ 8/ 1815 alipoanziasha shirika la wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu. Ndoto hiyo hadi sasa inaendelea maana shirika limesambaa na linaendelea kusambaa katika nchi nyingi duniani.Wamisionari walipofika hapa Tanzania mwaka 1966 walianza kazi ya kueneza upendo wa Damu ya Yesu. Mwaka 1990, nao walikuwa na ndoto ya kujenga seminari ili kuendeleza kwa urahisi kazi ya kupeleka upendo wa Damu ya Yesu. Leo tunapoadhimisha jubilei ya miaka 25 ya seminari hii, tunashuhudia kweli kweli kuwa NDOTO INAENDELEA.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa; Miaka ya 1990 kanisa la Tanzania lilianza kupata miito mingi kiasi kwamba Seminari kuu za (Kipalala, Peramiho, na Segerea) zilikuwa hazitoshi. Ndiyo maana (kama taarifa ya Pd. Francis Bartoloni inavyosema) mashirika mengi yalikuwa yanakosa nafasi na hivyo kupelekea kutuma vijana nchi za nje kwa masomo ya Taalimungu. Mahangaiko na ugumu wa kupeleka vijana nchi za nje hayajawahi kuwa rahisi tangu zamani hizo. Hata leo, kumpeleka kijana masomoni Ulaya au Amerika ni kazi sana hasa kupata nyaraka stahiki kama viza nk.(Wengi wamekuwa wakisema – pengine ni rahisi kupata viza ya kwenda mbinguni kuliko kwenda nchi za Ulaya na Amerika).Sambamba na hilo, kupeleka waseminari kusoma masomo ya MSINGI (Falsafa na Teolojia) nje ya mazingira watakayofanyia kazi ni hatari kwa ufanisi wa wito wao.Katika mazingira hayo wakubwa wetu waliota ndoto kuwa siku moja wangeachana na adha za namna hiyo.
Wakuu wa Mashirika ya kitawa, katika mikutano yao, walianza mjadala juu ya kujitegemea kimalezi. Wasalvatoriani chini ya Provincial wao Fr Andrea Urbansky walijitokeza na kuahidi kujenga shule ya taalimungu tu iwapo mashirika mengine yangewaunga mkono kwa kuleta wanafunzi na hata walimu. Kwa kuwa wasalvatoriani walikuwa wajenge Seminari kuukwa Taalimungu, tatizo lilibaki kwa Falsafa.Maamuzi yalifikiwa kuwa chuo cha falsafa kijengwe Dodoma.
Wakati Seminari hii inajengwa, Provinshowawakati huo alikuwa Pd. Beniamino Conti C.PP.S. Huyu alifanya maamuzi makubwa.Alikubali ombi la ujenzi wa Seminari mbil; ya Filosofia huko Dodoma na ya Taalimungu hapa Morogoro. Kama ilivyokwisha semwa, wasalvatoriani walipoamua kujenga na kuanza na falsafa, mkutano wa Business Assembly uliamua kufuta seminari ya Dodoma na kuongezanguvu kujenga hapa Morogoro kwa ajili ya Falsafa na Teologia.
Mwaka 1991 Pd. Beniamino alimaliza muda wake na Pd. Pietro Battista alichaguliwa na aliendeleza kazi iliyokuwa inaendelea. Alipokuja Tanzania alienda eneo la ujenzi, akaliangalia sana na akasema: (Hapa ndipo/mahali hapa ndipo) akimaanisha - Mahali hapa Bwana atatukuzwa. Alipapenda na akapabariki. Ndiyo maana nyumba hii imekuwa na mafanikio mazuri kwa miaka yote. Mwenyezi Mungu wa neema ametulinda na kutupigania kwa kila hali kwakuwa mahali hapa ndipo.
Wanafunzi wa kwanza kuhamia hapa
Baada ya ujenzi kukamilika mwaka 1993, mambo yote yalikuwa tayari isipokuwa tu changamoto ya maji ambayo Padre Francis Bartoloni amesimulia jinsi ilivyotatuliwa. Kabla ya kuitatua, mhula wa masomo ulianza na hivyo tarehe 15 Augusti 1993 siku ya maadhimisho ya 178 ya kuanzishwa shirika letu, waseminari wa kwanza walifika ikabidi waishi katika jumuya ya Wasalvatoriani kwa muhula moja. Wakati huo, Pd. Francis Bartoloni aliamua kuhamia hapa yeye na Mafrateri wawili wa mwaka wa kichungaji (Frt. Reginald Mrosso na Frt. Adolf Majetta) wakati ule, leo ni Pd. Majeta na Pd. Mrosso. Pamoja nao alikuwepo Br. Jerome Ng’itu Bosha aliyekuwa mkandidatiwa Ubruda wa mwaka ule. Leo ni baba wa familia. Waseminari waliokuwa walengwa (Falsafa) walihamia rasmi tarehe 7 Januari 1994na uzinduzi rasmi ulifanyika baadaye kwa nyakati tofauti kulingana na matukio, (Rej.Vita Nostra 6/1993, p.149).
Wanafunzi wa kwanza kabisa wa falsafa walioanza hapa walikuwa 13 na mlezi wao Pd. Francis Bartoloni, Gomberawa kwanza; kwa pamoja walikuwa 14. Mwaka wa masomo uliofuata 1994/95 liliingia kundi la pili la vijana waseminari wapatao 18, mwaka uliofuata 1995/96 vijana 8, na uliofuata 1997/1998vijana 5. Jumuiya ikaongezeka ikawa kubwa na woga ukaisha.Masomo ya Taalimungu yalianza rasmi katika Seminari kuu ya Wasalvatoriani (ambayo kwa sasa ni Jordan University College- JUCO). Kuanzia hapo makundi ya taalimunguna falsafa yaliendelea kuingia na kutoka kwa mtindo ambao umebaki hadi leo.
Ma-Gomberawa Seminari hii
Gombera wa kwanza alikuwa Pd. Francis Bartoloni ambaye ndiye aliyesimamia ujenzi wote. Tunathubutu kusema kuwa ndoto ya ujenzi huu aliibeba yeye, ndiye aliyebuni mtindo wa majengo yote na akamsimulia Msanifu wa majengo Mugendani ili aiweke kwenye makaratasi. Padre Francis alipenda nyumba zikae mbalimbali, lakini vyumba viwe karibu karibu ili kuwa pamoja zaidi. Tunaposema ndoto inaendelea ni pamoja na ndoto za namna hii. Yeye alikaa kwa miaka mitatu tu, tangu 1993 hadi 1996. Alifuata Pd. Vincent Boselli 1996 hadi 2000.Baadaye alifuata Pd. Gregory Mkhotya mwaka 2000 hadi 2004. Pd. Adolf Majeta kuanzia 2004 hadi 2006; Pd. Walter Milandu alianza 2006 hadi 2010. Akafuata Pd. Florence Kissima mwaka 2010 hadi Desemba 2016.Januari 2017 hadi sasa yuko Pd. Reginald Lyamuya, Mtumishi mwaminifu asiye stahali, ila kwa neema ya Mungu anaendelea.
Jubilei 2019
Jubilei maana yake nishangwe kwa sababu ni tukio linalofanyika mara moja kila baada ya miaka 25 au 50. Ni tukio la kufurahia sana. Tumesherekea Jubilei ya Seminari yetu. Nani anafurahia?Na anafurahia nini?
Malezi
Ni wazi kuwa tunasherekea maisha ya watu wote, waliolelewana kupata huduma za kitaaluma katika taasisi hii, mafanikio yaliyopatikana, uhai na furaha za watu wote wanaofaidika kwa huduma zinazotolewa na mamia ya watu waliopata huduma katika Seminari hii kwa miaka 25 iliyopita.
Kwa miaka 25 Seminari hii imefanikiwa kulea vijana zaidi ya 300 ambao wanatoa huduma zao ndani na nje ya Kanisa kwa uadilifu wa hali ya juu.Wanafunzi wapatao 205 wamesoma falsafa na 112 taalimungu. Idadi hiyo inaonekana kama ndogo kulinganisha na miaka 25 ya jubilee, lakini ieleweke kwamba ni namba kubwa sana kuzingatia kuwa kijana baada ya kidato cha 6 anakaa hapa akisoma kwa Miaka 9 ili apate shahadaya kwanza ya Falsafa na ya Taalimungu kwa Mujibu wa mafunzo ya Kanisa Katoliki.
Seminari hii ni kituo cha jamii ya watanzania, ni zawadi kubwa kwa kanisa na taifa la Tanzania kwa sababu watu waliopita hapa ni wa makundi mawili:
Makundi haya mawili ni ya vijana wavulana waliolelewa kwa misingi ya kuhudumu kwa uadilifu na uaminifu wa hali ya juu. Waliofanikiwa kuwa wamisionari ni 80; ndio wale waliotumwa kwenda kutoa huduma kwa jamii. Kama mapadre na mabruda, wanasimamia shughuli za kanisa kwa jamii kiroho na kimwili. Taasisi zote tunazoendesha (Hospitali, shule, maji kwa jamii na huduma za upendo zinapata wahudumu kutokakatika chuo hiki. Kundi la pili niwengine wote waliobaki ambao ni waamini wazuri na waadilifu na watendaji kazi wazuri.
Sote kwa pamoja tunamshukuru Mungu kwa kuwa sisi sote tuliosoma hapa tumefaidika binafsi, lakini hasa zaidi wengi wenye familia, wanajenga familia nzuri kutokana na malezi waliopata hapa. Wengi walio na wadhifa serikalini kama watumishi wamekuwa wakituletea sifa kubwa sana maana wanaonekana jinsi wanavyopendwa kutokana na uadilifu wao kazini.
Seminari hii Leo
Tunamshukuru Mungu kwa kuwa Seminari yetu leo inawaseminari 49, hao ni Waseminari wa Falsafa mwaka wa kwanza hadi wa 3 na Waseminari wa Taalimungu mwaka wa kwanza hadi wa 4. Makundi mengine ya vijana walioko kwenye miaka ya malezi maalum kama (Mwaka wa kwanza wa Malezi hukoDodoma, Mwaka wa Pili wa Malezi huko Singida na Mwaka wa uchungaji) hawahesabiwi katika kundi hilo.
Malezi yetu
Mpango na mtindo wetu wa malezi katika nyumba hii umesimama katika tasaufi yetu, maarufu kama (Tasaufi ya Damu Azizi) ambayo ina nguzo tatu.
Kwa kujitahidi kutimiza malengo hayo, jumuiya yetu imeunganisha tunu mbalimbali za kimalezi za waasisi wetu (Mt Gaspari) na za wataalamu waliobobea katika malezi ya vijana (Mt Don Bosco n.k) na kujiimarisha katika malezi yanayoongozwa na Upendo kuliko sheria, kwa neno La Kitaliano lililoko katika nembo yetu ya Jubilei AMOREVOLE jinsi linavyoeleweka nakutumika katika mitindo ya malezi ya Mt. Don Bosco. Malezi ya namna hii yamesaidia sana jumuiya yetu kuunda vijana waliokomaa katika nyanja zote. Tunaposema tumepata sifa nyingi toka taasisi mbalimbali za kiserikali na kidini, zenye kupongeza huduma zetu, ni kwa ajili ya mtindo wa malezi unaofumbatwa katika kifungo cha upendo lakini zaidi sana katika tasaufi ya Damu ya Yesu. Watu hufanya kazi kwa juhudi, kwa kiwango na vizuri kwa kujitoa hadi tone la mwisho.
Hitimisho
Mafanikio ya Seminari yetuni juhudi za watu wengi; Magombera waliopita na walezi wasaidizi wamekuwa pamoja katika kutekeleza yote. Natambua kuwa bila mazoezi, mchezaji anapoteza kipaji chake. Maisha ya tasaufi tuliyojifunza na tunayoendela kuishi yanapaswa kuwa tabia ili tunu hizi zisipotee.Tunaomba sala zenu ili sisi tunaofanya kazi hii ya kuwaanda wahudumu wa Kanisa na wa taifa, tusikosee, bali tufuate misingi bora kwa manufaa ya Kanisa, taifa na vijana wenyewe.